Tuesday, 24 April 2007

Baada ya ajari kuongezeka vidhibiti mwendo vyakumbukwa

Chama cha wamiliki wa mabasi nchini-TABOA kimewaagiza wamiliki wa mabasi yote kuhakikisha kuwa mabasi yao yana vidhibiti mwendo vinavyofanyakazi.
Kimesema wakati serikali inafanya jitihada za kutafuta njia mbadala ya kudhibiti mwendo kasi vidhibiti mwendo vilivyopo kwenye mabasi kwa sasa ndio viendelee kutumika.
Agizo hilo limetolewa Mjini DAR ES SALAAM na Mwenyekiti wa Taifa wa TABOA Bwana MOHAMMED ABDULLAH mara baada ya kukutana na Makamanda wa usalama barabarani wa mikoa yote nchini kwa lengo la kubadilishana mawazo juu ya kuboresha usafirishaji wa abiria.
Katika taarifa yake Bwana ABDULLAH pia amewaagiza abiria wa mabasi hayo kumkemea dereva anayeendesha vibaya ikiwa ni pamoja na kwenda mwendo wa kasi.
Amesema, endapo dereva huyo atakaidi, watoe taarifa ya dereva huyo kwa mmiliki wa basi au kwa polisi wa usalama barabarani.
Mwenyekiti huyo wa chama cha wamiliki wa mabasi nchini amewashauri abiria wote nchini kuwa na utamaduni wa kudai tiketi inayoonyesha nauli anayotozwa, namba ya kiti, sehemu atokayo na aendayo.
Bwana ABDULLAH amesema, endapo kutakuwa na ushirikiano kati ya abiria, wamiliki wa mabasi na askari wa usalama barabarani, usafiri kwa njia ya barabara utaimarishwa na hivyo kupunguza ajali za barabarani.

No comments: